MZEE GURUMO NA DIAMOND

AMA kweli ajuaye siku ya binadamu kufa ni
Mungu peke yake , kama wanadamu nao
wangepewa uwezo huo, kuna mipango
ingekuwa haipangwi kwa kujua haitatimia ,
ndivyo ilivyotokea kwa marehemu Muhidin
‘ Maalim ’ Gurumo ambaye ameaga dunia
akiwa na zawadi aliyotaka kumpa Mbongo-
Fleva , Nasibu Abdul ‘ Diamond Platinumz ’ .
Marehemu Muhidin ‘ Maalim’ Gurumo wakati
akikabidhiwa ufunguo wa gari na msanii
Diamond Platnumz .
Gurumo alifariki dunia Aprili 13 , 2014 katika
Wadi ya Mwaisela Hospitali ya Taifa
Muhimbili jijini Dar na kuzikwa Aprili 15,
mwaka huu kwenye Makaburi ya Kijiji cha
Masaki, Kisarawe mkoani Pwani.
Zawadi ambayo marehemu Gurumo alikuwa
ampatie Diamond ni mashairi ya wimbo
ambao upo tayari na sasa , ilikuwa wakutane
na kukabidhiana tu .
ILIKUWA HIVI
Kwa mujibu wa Meneja wa Diamond , Babu
Tale ambaye alizungumza na Amani juzi
msibani nyumbani kwa Gurumo, Mabibo jijini
Dar , Ijumaa ya Aprili 11 , mwaka huu , mzee
huyo alimpigia simu ya mkononi yeye ( Babu
Tale) baada ya kumkosa Diamond .
Marehemu Muhidin ‘Maalim ’ Gurumo enzi za
uhai wake .
“Aliniuliza mwanangu ( Diamond ) yuko wapi ?
Nikamwambia yuko nje ya nchi . Akaniambia
nina zawadi nzuri sana nataka kumpa kabla
sijafa.“Nilimuuliza ni zawadi gani ? Akasema
ametunga wimbo, tayari umekamilika sasa
anataka kumpa aimbe yeye mwenyewe
( Diamond ) au waimbe wote.
“Niliona ni wazo zuri sana, nikamwambia kwa
sababu Diamond atarudi Jumapili , basi
Jumatatu tutakuja , akasema sawa asikose.
Sikujua kama anaumwa , sikujua kama
anazungumza na mimi maneno ya mwisho , ”
alisema Babu Tale ambaye kwa kiasi kikubwa
ameshiriki kumwinua kisanii Diamond .
DIAMOND APIGIWA SIMU , AFURAHIA
Babu Tale aliendelea kusema kuwa , baada ya
kumaliza kuzungumza na mzee Gurumo
alimpigia simu Diamond ambapo alimwambia
kilichosemwa na mzee huyo.
“Nilimpigia simu Diamond baada ya kukata
kwa mzee Gurumo , nikamwambia alichosema
mzee wake. Sikujua kama Diamond
angefurahi sana , lakini kusema kweli alifurahi
sana tena sana akasema mzee ametoa wazo
zuri ambalo litamwingiza kwenye historia
nyingine kwa vile atakuwa ameimba na
mkongwe wa muziki Tanzania .
Mbongo- Fleva, Nasibu Abdul alimaarufu
‘ Diamond Platinumz ’.
DIAMOND ASHTUKA , AKIONA KIFO CHA
GURUMO
Babu Tale akaendelea : “Lakini cha ajabu ,
Diamond akawa kama ameshtuka , akasema
da! Huyo mzee ametoa wazo zuri namna
hiyo ? Au anataka kufa nini?”
Meneja huyo aliendelea kusema kuwa , baada
ya hapo hakuwa na mawasiliano tena na
mzee Gurumo hadi Jumapili, siku mbili mbele
baada ya tamko la kumpa Diamond zawadi
ya wimbo ambapo alipigiwa simu na mtu
akimwambia mzee Gurumo amefariki dunia .
Anasema : “Najua Gurumo alitaka kumpa
Diamond wimbo huo kama zawadi yake na
yeye kufuatia Diamond kumzawadia gari
( Toyota FunCargo ) alilomkabidhi mwaka jana
kwa ‘ kumsapraizi ’ . ”
JINA LA WIMBO
Babu Tale hakutaja jina la wimbo huo lakini
fukuafukua ya Amani iliambiwa kuwa , wimbo
ambao Gurumo alitaka kumpa Diamond
unaitwa Shukurani kwa Mtoto .
Amani lilifanya jitihada za kuzungumza na
mtoto yeyote wa marehemu ili kujua kama
kuna mwenye kuelewa kuhusu wimbo huo na
kama mashairi yake yanaweza kupatikana ,
lakini bila mafanikio baada ya watoto wote
kuwa katika majonzi yasiyopimika kwa
kiwango cha macho ya kibinadamu .
Gari aina ya Toyota FunCargo alilopewa
marehemu Gurumo ikiwa ni zawadi kutoka
kwa Diamond.
DIAMOND AANGUA KILIO KAMA MTOTO
Habari nje ya Babu Tale zinadai kuwa ,
Diamond alipojulishwa juu ya kifo cha mzee
Gurumo aliangua kilio kama mtoto mdogo .
Inadaiwa kuwa , staa huyo aliyekuwa nchini
Nigeria kwa shoo kadhaa, alikuwa akilia huku
akikumbuka maneno ya Babu Tale kuhusu
kuimba wimbo na mzee huyo ambaye
Jumatatu ya kukutana kwao ndiyo mwili
wake ulikuwa Mochwari ya Hospitali ya
Muhimbili jijini Dar .
“Diamond alilia huku akisema kuwa ameikosa
bahati moja kubwa sana na hatakuja kuipata
tena katika maisha yake. Unajua yeye
alikubali wazo la Gurumo akijua ni ‘ kiki ’ ya
kuendelea kufanya vyema kwenye gemu, ”
kilisema chanzo kimoja.
Jitihada za kumpata Diamond ambaye
alikosa kuhudhuria mazishi ya mzee Gurumo
zilishindikana baada ya simu yake ya
kiganjani kuita bila kupokelewa. Hata
alipotumiwa ujumbe mfupi hakuujibu .
Marehemu Gurumo akiwa kwenye gari lake .
GURUMO ANAHITIMISHA SAFU YA
WAIMBAJI MSONDO
Kifo cha Maalim Gurumo kinahitimisha safu
ya waimbaji wakongwe wa kwenye Bendi ya
Msondo Music . Waimbaji wengine
waliotangulia mbele ya haki ni Suleiman
Mbwembwe , TX Moshi William , Athuman
Momba na Joseph Maina .
Wote hawa ndiyo walioimba wimbo maarufu
wenye mashairi yasemayo ‘ tunatoana roho
yarabi iii … kwa mali alizoacha baabaa ’ .. .
Ukiiangalia video ya wimbo huo , waimbaji
wote ni marehemu. Inauma sana !
Marehemu Gurumo alizikwa juzi `Jumanne
kwenye Makaburi ya Kijiji cha Masaki,
Kisarawe Pwani.
Mungu ailaze roho yake mahali pema
peponi. Amina .

0 comments:

Post a Comment