R.I.P GURUMO

MWANAMUZI nguli wa muziki wa dansi
nchini , Muhidini Maalim Gurumo
aliyefahamika pia kama kamanda na
mashabiki wa muziki wa dansi, aliyeaga
dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya
Muhimbili jijini Dar , alikutana na mateso ya
kwa saa 72 za mwisho wake baada ya
kulazwa akiwa taabani kwa siku tatu .
Mwanamuziki Muhidini Maalim Gurumo
akiwa mahututi katika hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Mtoto wa marehemu anayejulikana kwa jina
la Abdalah aliliambia gazeti hili kuwa siku
mauti yalipomfika baba yake katika wodi
namba sita Jengo la Mwaisela, alimtembelea
na kumkuta akiwa katika hali nzuri na
alipopewa chakula alikula , akashiba lakini
cha ajabu alisema hatakula tena .
Kijana huyo alisema muda mfupi baadaye,
hali ya baba yake ilibadilika , akaanza
kupumua kwa shida ndipo alipozidiwa na
baadaye kukata roho.
Maalim Gurumo akiwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kabla ya kufikwa na mauti .
Mzee Gurumo alikuwa akisumbuliwa na
ugonjwa wa mapafu kwa muda mrefu na
aliwahi kulazwa katika hospitali hiyo ya
Muhimbili .
Baadhi ya watu waliomtembelea mzee
Gurumo kwa nyakati tofauti akiwa hospitalini
hapo ni pamoja na Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania , Dk . Jakaya Mrisho
Kikwete ambaye alimuombea afya njema na
akaruhusiwa kurudi nyumbani .
Mzee Gurumo akiimba wakati wa uhai wake.
Kifo chake kimeacha simanzi si tu kwa
familia yake, bali kwa wadau wa muziki wa
dansi kwani alikuwa mwalimu na kiongozi wa
wanamuziki wengi ambao sasa wanatamba.
Baada ya kustaafu muziki , Mzee aliwahi
kupewa zawadi ya gari na msanii wa Bongo
Fleva , Naseeb Abdul ‘ Diamond Platnumz ’
aina ya Toyota Funcargo.
Akizungumzia msiba huo, Kiongozi wa Bendi
ya Extra Bongo, Ally Choki alisema
wamempoteza mwalimu wa muziki
asiyekuwa na choyo ya kuelimisha .
Mzee Gurumo akiwa na mkewe.
“Ni kama tumepoteza tochi tukiwa kwenye
msitu mnene usiku wa manane , ” alisema .
Naye msemaji wa Bendi ya Mlimani Park
Ochestra ( Sikinde Ngoma ya Ukae) , Jimmy
Chika alipozungumza na gazeti hili alisema
mzee Gurumo aliwahi kuja kuwatembelea na
kuimba mwezi mmoja uliopita katika Ukumbi
wa DDC , Kariakoo jijini Dar .
“Alikuja kama mara tatu hivi ukumbini, naona
alikuwa kama anatuaga kwa sababu alikuwa
mwanzilishi wa bendi na mbunifu wa mtindo
wa Sikinde, aliubuni Septemba , 1978 , ”
alisema Chika .Mzee Kassim Mapili ,
mwanamuziki wa mkongwe , kwa upande
wake alisema kifo cha Gurumo ni pengo
kubwa ambalo haliwezi kuzibika na
akafafanua kuwa ni mtu ambaye hakuwa
mbinafsi.
Mzee Gurumo akiwa na CD yenye nyimbo
zake .
Baadhi ya wanamuziki ambao amefanya nao
kazi kwa karibu ambao sasa watakuwa
wanamlilia mwalimu wao ni pamoja na
Hassan Rehani Bitchuka , Said Mabela ,
Roman Mng ’ ande ‘ Romario ’ na wengine
wengi.
Gurumo pia ameacha simanzi katika miji
mbalimbali nchini kwa kuwa amewahi
kutembelea kimuziki na alifanikiwa kujizolea
mashabiki lukuki .
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni msiba
ulikuwa nyumbani kwake Mabibo , Dar huku
taratibu za mazishi zikifanyika. Ameacha
mjane na watoto wanne .
Mungu ailaze roho ya marehemu maali pema
peponi. Amina .

0 comments:

Post a Comment